Berean Christadelphians

Masomo ya Kila Siku

-main-

exo 35

1Musa akakutanisha mkutano wote wa wana wa Israeli,
na kuwaambia,
Maneno aliyoyausia Bwana ni haya,
kwamba myafanye.
2Fanyeni kazi siku sita,
lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu;
ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa Bwana;
mtu awaye yote atakayefanya kazi yo yote katika siku hiyo atauawa.
3Hamtawasha moto katika nyumba zenu kwa siku ya Sabato.
4Kisha Musa akanena na mkutano wote wa wana wa Israeli,
akawaambia,
Neno hili ndilo aliloliamuru Bwana,
akisema,
5Katwaeni kati yenu matoleo kwa Bwana;
mtu awaye yote aliye na moyo wa kupenda,
ayalete matoleo;
dhahabu na fedha na shaba;
6na nyuzi za rangi ya samawi,
na za rangi ya zambarau,
na za rangi nyekundu,
na kitani nzuri,
na singa za mbuzi;
7na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu,
na ngozi za pomboo,
na mbao za mshita;
8na mafuta kwa hiyo taa,
na viungo vya manukato kwa hayo mafuta ya kutiwa,
na kwa huo uvumba mzuri;
9na vito vya shohamu,
na vito vya kutiwa kwa hiyo naivera,
na kwa hicho kifuko cha kifuani.
10Na kila mtu kati yenu aliye na moyo wa hekima na aje,
na kuyafanya hayo yote ambayo Bwana ameyaagiza;
11yaani,
hiyo maskani na hema yake,
na kifuniko chake,
na vifungo vyake,
na mbao zake,
na mataruma yake,
na viguzo vyake,
na matako yake;
12hilo sanduku,
na miti yake,
na hicho kiti cha rehema,
na lile pazia la sitara;
13na hiyo meza,
na miti yake,
na vyombo vyake vyote,
na hiyo mikate ya wonyesho;
14na hicho kinara cha taa kwa mwanga,
na vyombo vyake,
na taa zake,
na hayo mafuta kwa nuru;
15na hiyo madhabahu ya kufukizia uvumba,
na miti yake,
na hayo mafuta ya kupaka,
na huo uvumba mzuri,
na hicho kisitiri cha mlango,
mlangoni mwa hiyo maskani;
16na hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa,
pamoja na wavu wake wa shaba,
na miti yake,
na vyombo vyake vyote,
na hilo birika na tako lake;
17na hizo kuta za nguo za ua,
na viguzo vyake,
na matako yake,
na pazia la lango la ua;
18na vile vigingi vya maskani,
na vigingi vya ua,
na kamba zake
19na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri,
kwa ajili ya kutumika ndani ya mahali patakatifu,
hayo mavazi matakatifu ya Haruni kuhani,
na mavazi ya wanawe,
ili kutumika katika kazi ya ukuhani.
20Basi mkutano wote wa wana wa Israeli wakaondoka hapo mbele ya Musa.
21Wakaja kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza,
na kila mtu ambaye roho yake ilimfanya kuwa apenda,
nao wakaleta sadaka za kumpa Bwana,
kwa kazi ya hema ya kukutania,
na kwa utumishi wake,
na kwa hayo mavazi matakatifu.
22Nao wakaja,
waume kwa wake,
wote waliokuwa na moyo wa kupenda,
wakaleta vipini,
na hazama,
na pete za muhuri,
na vikuku,
na vyombo vyote vya dhahabu;
kila mtu aliyetoa toleo la dhahabu la kumpa Bwana.
23Tena kila mtu aliyeona kwake nyuzi za rangi ya samawi,
na nyuzi za rangi ya zambarau,
na nyekundu,
na kitani nzuri,
na singa za mbuzi,
na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu,
na ngozi za pomboo,
akavileta.
24Kila mtu aliyetoa toleo la fedha,
na la shaba,
akaileta sadaka ya Bwana;
na kila mtu,
aliyeona kwake mti wa mshita kwa kazi yo yote ya huo utumishi,
akauleta.
25Na wanawake wote waliokuwa na mioyo ya hekima,
walisokota kwa mikono yao,
nao wakaleta hizo walizokuwa wamezisokota,
nguo za rangi ya samawi,
na za rangi ya zambarau,
na hizo nyuzi nyekundu,
na hiyo nguo ya kitani nzuri.
26Na wanawake wote ambao mioyo yao iliwahimiza katika hekima wakasokota hizo singa za mbuzi.
27Na hao wakuu wakavileta vile vito vya shohamu,
na vito vya kutiwa,
kwa hiyo naivera,
na kwa hicho kifuko cha kifuani,
28na viungo vya manukato,
na mafuta;
kwa hiyo taa,
na kwa hayo mafuta ya kutiwa,
na kwa huo uvumba mzuri.
29Wana wa Israeli wakaleta sadaka za kumpa Bwana kwa moyo wa kupenda;
wote,
waume kwa wake,
ambao mioyo yao iliwafanya kuwa wapenda kuleta kwa hiyo kazi,
ambayo Bwana aliamuru ifanywe kwa mkono wa Musa.
30Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli,
Angalieni,
Bwana amemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri,
mwana wa Huri,
wa kabila ya Yuda;
31naye amemjaza roho ya Mungu,
katika hekima,
na akili,
na ujuzi,
na kazi ya ustadi kila aina;
32na kuvumbua kazi za werevu,
na kufanya kazi ya dhahabu,
na fedha,
na shaba,
33na kukata vito vya kutilia,
na kuchora miti,
atumike katika kazi za werevu kila aina.
34Naye amemtilia moyoni mwake ili apate kufundisha,
yeye,
na Oholiabu mwana wa Ahisamaki,
wa kabila ya Dani.
35Amewajaza watu hao akili za moyoni,
ili watumike katika kazi kila aina,
ya mwenye kuchora mawe,
na kazi ya werevu,
na ya mwenye kutia taraza,
katika nyuzi za rangi ya samawi,
na za rangi ya zambarau,
na nyekundu,
na kitani nzuri,
na ya mwenye kufuma nguo;
ya hao wafanyao kazi yo yote,
na ya wenye kuvumbua kazi za werevu.

psa 92

1Ni neno jema kumshukuru Bwana,
Na kuliimbia jina lako,
Ee Uliye juu.
2Kuzitangaza rehema zako asubuhi,
Na uaminifu wako wakati wa usiku.
3Kwa chombo chenye nyuzi kumi,
Na kwa kinanda,
Na kwa mlio wa kinubi.
4Kwa kuwa umenifurahisha,
Bwana,
Kwa kazi yako;
nitashangilia Kwa ajili ya matendo ya mikono yako.
5Ee Bwana,
jinsi yalivyo makuu matendo yako!
Mawazo yako ni mafumbo makubwa.
6Mtu mjinga hayatambui hayo,
Wala mpumbavu hayafahamu.
7Wasio haki wakichipuka kama majani Na wote watendao maovu wakistawi.
Ni kwa kusudi waangamizwe milele;
8Bali Wewe,
Bwana,
U Mtukufu hata milele.
9Maana hao adui zako,
Ee Bwana,
Hao adui zako watapotea,
Na watendao maovu watatawanyika wote pia.
10Bali pembe yangu umeiinua kama pembe ya nyati,
Nimepakwa mafuta mabichi.
11Na jicho langu limewatazama walioniotea,
Sikio langu limesikia habari za waovu walionishambulia.
12Mwenye haki atasitawi kama mtende,
Atakua kama mwerezi wa Lebanoni.
13Waliopandwa katika nyumba ya Bwana Watasitawi katika nyua za Mungu wetu.
14Watazaa matunda hadi wakati wa uzee,
Watajaa utomvu,
watakuwa na ubichi.
15Watangaze ya kuwa Bwana ni mwenye adili,
Mwamba wangu,
ndani yake hamna udhalimu.

psa 93

1Bwana ametamalaki,
amejivika adhama,
Bwana amejivika,
na kujikaza nguvu.
Naam,
ulimwengu umethibitika usitikisike;
2Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani;
Wewe ndiwe uliye tangu milele.
3Ee Bwana,
mito imepaza,
Mito imepaza sauti zake,
Mito imepaza uvumi wake.
4Kupita sauti ya maji mengi,
maji makuu,
Kupita mawimbi ya bahari yaumkayo,
Bwana Aliye juu ndiye mwenye ukuu.
5Shuhuda zako ni amini sana;
Utakatifu ndio uifaao nyumba yako,
Ee Bwana,
milele na milele.

1co 4

1Mtu na atuhesabu hivi,
kuwa tu watumishi wa Kristo,
na mawakili wa siri za Mungu.
2Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili,
ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu.
3Lakini,
kwangu mimi,
si kitu kabisa nihukumiwe na ninyi,
wala kwa hukumu ya kibinadamu,
wala sijihukumu hata nafsi yangu.
4Maana sijui sababu ya kujishitaki nafsi yangu,
lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo;
ila anihukumuye mimi ni Bwana.
5Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake,
hata ajapo Bwana;
ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza,
na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo;
ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu.
6Basi ndugu,
mambo hayo nimeyafanya kuwa mfano wa mimi na Apolo kwa ajili yenu,
ili kwamba kwa mfano wetu mpate kujifunza kutokupita yale yaliyoandikwa;
ili mmoja wenu asijivune kwa ajili ya huyu,
kinyume cha mwenziwe.
7Maana ni nani anayekupambanua na mwingine?
Nawe una nini usichokipokea?
Lakini iwapo ulipokea,
wajisifia nini kana kwamba hukupokea?
8Mmekwisha kushiba,
mmekwisha kupata utajiri,
mmemiliki pasipo sisi.
Naam,
laiti mngemiliki,
ili sisi nasi tumiliki pamoja nanyi!
9Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho,
kama watu waliohukumiwa wauawe;
kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia;
kwa malaika na wanadamu.
10Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo,
lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo;
sisi tu dhaifu,
lakini ninyi mna nguvu;
ninyi mna utukufu,
lakini sisi hatupati heshima.
11Hata saa hii ya sasa,
tuna njaa na kiu,
tu uchi,
twapigwa ngumi,
tena hatuna makao;
12kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe.
Tukitukanwa twabariki,
tukiudhiwa twastahimili;
13tukisingiziwa twasihi;
tumefanywa kama takataka za dunia,
na tama ya vitu vyote hata sasa.
14Siyaandiki hayo ili kuwatahayarisha;
bali kuwaonya kama watoto niwapendao.
15Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo,
walakini hamna baba wengi.
Maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.
16Basi,
nawasihi mnifuate mimi.
17Kwa sababu hii nimemtuma Timotheo kwenu,
aliye mwanangu mpendwa,
mwaminifu katika Bwana,
atakayewakumbusha njia zangu zilizo katika Kristo,
kama vile nifundishavyo kila mahali katika kila kanisa.
18Basi wengine wamejivuna kana kwamba siji kwenu.
19Lakini nitakuja kwenu upesi,
nikijaliwa,
nami nitafahamu,
si neno lao tu waliojivuna,
bali nguvu zao.
20Maana ufalme wa Mungu hauwi katika neno,
bali katika nguvu.
21Mnataka vipi?
Nije kwenu na fimbo,
au nije katika upendo na roho ya upole?

1co 5

1Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa,
na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa,
kwamba mtu awe na mke wa babaye.
2Nanyi mwajivuna,
wala hamkusikitika,
ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo.
3Kwa maana kweli,
nisipokuwapo kwa mwili,
lakini nikiwapo kwa roho,
mimi mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo,
kana kwamba nikiwapo.
4Katika jina la Bwana wetu Yesu,
ninyi mkiwa mmekusanyika pamoja na roho yangu,
pamoja na uweza wa Bwana wetu Yesu;
5kumtolea Shetani mtu huyo,
ili mwili uadhibiwe,
ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana Yesu.
6Kujisifu kwenu si kuzuri.
Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima?
7Basi,
jisafisheni,
mkatoe ile chachu ya kale,
mpate kuwa donge jipya,
kama vile mlivyo hamkutiwa chachu.
Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka,
yaani,
Kristo;
8basi na tuifanye karamu,
si kwa chachu ya kale,
wala kwa chachu ya uovu na ubaya,
bali kwa yasiyochachika,
ndio weupe wa moyo na kweli.
9Naliwaandikia katika waraka wangu,
kwamba msichangamane na wazinzi.
10Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii,
au na wenye kutamani,
au na wanyang'anyi,
au na wenye kuabudu sanamu;
maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia.
11Lakini,
mambo yalivyo,
naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu,
akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi;
mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.
12Maana yanihusu nini kuwahukumu wale walio nje?
Ninyi hamwahukumu hao walio ndani?
13Lakini hao walio nje Mungu atawahukumu.
Ninyi mwondoeni yule mbaya miongoni mwenu.