Kristadelfiani (ndugu na dada katika Kristo) walikuja kujulikana kwa jina hili karne moja iliyopita, lakini lengo lao ni kuishi kwa imani katika Yesu Kristo, kwa kuambatana na mafundisho ya wafuasi wake tokea karne ya kwanza, wakipata maelezo yao kutoka katika Biblia.
Wanaamini ya kuwa wale wanaomfuata Yesu na mitume wake sasa, wakimtazamia kwa nguvu na msamaha kutoka kwa Mungu waweza kuweka tumaini lao kwa kuja kwake tena duniani atakapouleta uzima wa milele kwa watu wake, na aimarishe kwa nguvu ufalme wa Mungu ulioahidiwa tangu zamani.
Maelezo yaliyomo katika kijitabu hiki ni ubishi
makusudi ukimuuliza kila msomaji kulinganisha nia au mawazo yake
na mafunzo wazi ya Maandiko, akichungua kwa makini vifungu vya
Biblia vinavyoonyesha ushahidi. Ikiwa, kama matokeo, kuna ugeuzo
wa mawazo na moyo unashawishika, hakutakuwa na shaka kuwa mafundisho
ya Bwana, na kitabu alichokiamini ni lazima kifuatwe po pote kinapoongoza.
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo tunapaswa kuamini maandiko
kabisa kama Yesu na Mitume wake walivyofanya:
Yesu: "Maandiko hayawezi
kutanguka" (Yohana 10:35).
Paulo: "Kila andiko,
lenye pumzi ya Mungu lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaongoza,
na kwa kuwaadibisha katika haki" (2 Timotheo 3:16)
Petro: "Maana unabii
haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena
yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu" (2 Petro
1:21)
Petro: "Mambo hayo
ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili
kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni" (1 Petro 1:12).
Imani ya kweli lazima iwe na msingi juu ya Biblia.
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo tunapaswa kukubali
kuwa tu wenye dhambi na viumbe vya kufa bila tumaini la uzima
isipokuwa katika Kristo:
Musa: "U mavumbi
wewe, nawe mavumbini utarudi" (Mwanzo 3:19).
Zaburi: "Msiwatumainie
wakuu, wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake. Pumzi yake hutoka,
huurudia udongo wake, siku hiyo mawazo yake yapotea" (Zaburi
146:3, 4).
Isaya: "Wote wenye
mwili ni majani, na wema wake wote ni kama ua la kondeni; majani
yakauka, ua lanyauka" (Isaya 40:6, 7).
Yakobo: "Uzima wenu
ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka"
(Yakobo 4:14).
Petro: "Mwili wote
ni kama majani, na fahari yake yote ni kama ua la majani. Majani
hukauka na ua lake huanguka" (1 Petro 1:24).
Biblia yaonyesha wazi kuwa sisi tu viumbe vya kufa:
tukikiri hivi, hapo twaweza kutazamia wokovu tulioahidiwa.
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo twapaswa kukubali kuwa
kipawa chetu kitazamiwe nchini na wala sio mbinguni:
Zaburi: "Bali wenye
upole watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani"
(Zaburi 37:11, Mathayo 5:5).
Yesu: "Ukawafanya
kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya
nchi" (Ufunuo 5:10).
Danieli: "Jiwe lilioipiga hiyo sanamu likawa mlima mkubwa likaijaza dunia yote . . . Na katika siku za wafalme hao Mungu wa Mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele" (Danieli 2:35, 44; 7:27).
Zaburi: "Mbingu ni
mbingu za Bwana, bali nchi amewapa wanadamu" (Zaburi 115:16).
Yohana: "Wala hakuna
mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani
mwana wa Adamu" (Yohana 3:13).
Biblia yatwambia kuwa kipawa au urithi umewekwa
mbinguni kwa sasa pamoja na Kristo, utafunuliwa nchini ajapo:
Petro: "Urithi usioharibika,
usio na uchafu, usionyauka uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu
. . . mpate wokovu tayari kufunuliwa wakati wa mwisho . . . mkiitumainia
kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu
Kristo" (1 Petro 1:4, 5, 13).
Paulo: "Kwa maana
sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia
Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge"
(Wafilipi 3:20, 21).
Biblia yatwambia kuwa Mungu alimweka mwanadamu katika
nchi (duniani) hapo mwanzo kabisa alipomwumba. Naye binadamu atapokea
baraka zake mwenyezi Mungu akiwa papa hada duniani, sio kwingine.
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo twapaswa kutambua kuwa
kaburi ni mahali pa kutokuwa na ufahamu wo wote, ambao ufufuo
tu waweza kuumaliza:
Zaburi: "Maana mautini
hapana kumbukumbu lako; katika kuzimu ni nani atakayekushukuru?"
(Zaburi 6:5).
Hezekia: "Kwa kuwa
kuzimu hakuwezi kukusifu; mauti haiwezi kukuadhimisha; wale washukao
shimoni hawawezi kuitarajia kweli yako" (Isaya 38:18).
Petro: "Daudi . .
. alifariki akazikwa, na kaburi lake liko kwetu hata leo . . .
Maana Daudi hakupanda mbinguni" (Matendo 2:29, 34).
Paulo: "Na Kama Kristo
hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu.
Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika
maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu
wote" (1 Wakorintho 15: 17-19).
Kaburi, na "hell" (kuzimu) iliyo katika
Agano la kale, ni neno moja na mahali pamoja. Hapa ndipo waendako
wanaokufa wote.
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo twapaswa kujiunga pamoja
na wanafunzi wa kwanza katika kutazamia kuja kwake mara ya pili:
Yesu: "Atakapokuja
Mwana wa Adamu katika utukufu wake na malaika watakatifu wote
pamoja naye" (Mathayo 25:31).
Malaika: "Huyu Yesu
aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi
iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni" (Matendo 1:11).
Petro: "Apate (Mungu)
kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani" (Matendo 3:20).
Paulo: "Kwa sababu
Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na
sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu" (1 Wathesalonike
4:16).
Ni kwa kuja mara ya pili kwa Kristo ndiko kutakakoimaliza
kazi aliyoifanya alipokuja hapa mara ya kwanza.
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo tutakuwa na hakika
kuwa Bwana wetu Yesu Kristo, atakaporudi, atakuwa Mfalme nchini
mwote:
Gabrieli: "Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi; baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho" (Luka 1:32-33).
Yesu: "Usiape kabisa
. . . kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu"
(Mathayo 5:35).
Yeremiah: "Tazama
siku zinakuja asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi chipukizi
la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya
hukumu na haki katika nchi. Katika siku zake Yuda ataokolewa,
Yuda na Israeli atakaa salama; na jina lake atakaloitwa ni hili,
Bwana ni haki yetu" (Yeremia 23:5, 6).
Zekaria: "Na siku
hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa Mizeituni. . . Naye
Bwana atakuwa Mfalme juu ya nchi yote; siku hiyo Bwana atakuwa
mmoja, na jina lake moja" (Zekaria 14:4, 9).
Paulo: "Kwa maana
(Mungu) ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa
mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo
haya kwa kumfufua kwa wafu" (Matendo 17:31).
Ni kwa utawala wa haki wa Yesu juu ya nchi utakaomwezesha
Mungu kuujaza ulimwengu kwa utukufu wake.
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo twaweza kufurahia ufahamu
kuwa Mungu ataimarisha Ufalme wake katika nguvu zake juu ya nchi:
Danieli: "Na katika
siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao
hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake;
bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao
utasimama milele na milele" (Danieli 2:44).
Yesu: "Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele . . . Tunakushukuru wewe, Bwana Mungu Mwenyezi uliyeko na uliyekuwako, kwa sababu umeutwaa uweza wako ulio mkuu, na kumiliki" (Ufunuo 11:15, 17).
Kwa kweli Mungu ndiye mtawala juu ya Ulimwengu wote:
Zaburi: "Bwana ameweka
kiti chake cha enzi mbinguni, na ufalme wake unavitawala vitu
vyote" (Zaburi 103:19).
Danieli: "Aliye juu
ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu naye humpa yeye amtakaye,
awaye yote . . . mamlaka yake ni mamlaka ya milele, na ufalme
wake hudumu toka kizazi hata kizazi" (Danieli 4:25, 34).
Hapo zamani aliimarisha Ufalme wake katika Israeli,
na akauondoa kwa ajili ya uovu wa watu wake:
Musa: "Ikiwa mtaitii
sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu . . . mtakuwa
kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu" (Kutoka 19:5,
6).
Daudi: "Uhimidiwe,
Ee Bwana, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele. Ee Bwana,
ukuu ni wako na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi; maana
vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; Ufalme ni wako,
Ee Bwana, nawe umetukuzwa u mkuu juu ya vitu vyote . . . Ndipo
sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Bwana awe mfalme badala
ya Daudi babaye, akafanikiwa" (1 Mambo ya Nyakati 29:10,
11, 23).
Ezekieli: "Na wewe,
Ewe mtu mwovu, ambaye siku yako imekuja, katika wakati wa uovu
wa mwisho; Bwana Mungu asema hivi; kiondoe kilemba, ivue taji
. . . Nitakipindua, nitakipindua, nitakipindua; hiki nacho hakitakuwa
tena hata atakapokuja yeye ambaye ni haki yake; nami nitampa"
(Ezekieli 21:25-27).
Yesu atakopoimarisha ufalme tena, Israeli walioasi
lazima watubu, na wasiotubu watakataliwa.
Zekaria: "Nao watamtazama yeye ambaye walimchoma, nao watamwombolezea kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee" (Zekaria 12:10; Tazama Ufunuo 1:7).
Yesu: "Ndipo kutakapokuwa
na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo
na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa
nje" (Luka 13:28).
Yesu ataimarisha ufalme wake kwa kushinda na kuangusha
mataifa yote na hata hivyo taifa lililomsulubisha litahitajika
kuwa chini yake.
Ikiwa twajidai kuwa wakristo tutakubali kuwa dhambi
hutokana na moyo wa mtu na hupatikana kwa mtu "Ibilisi"
aliye na uadui na Mungu:
Yeremia: "Moyo huwa
mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha" (Yeremia
17:9).
Yakobo: "Lakini kila
mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa"
(Yakobo 1:14).
Waebrania: "Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani Ibilisi" (Waebrania 2:14;)
Lakini sasa, mara moja tu, katika utimilifu wa nyakati,
amefunuliwa, azitangue dhambi kwa dhabihu ya nafsi yake"
(Waebrania 9:26).
Yesu: "Kwa maana
ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, usherati, wivi, uuaji,
uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano
kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia
mtu unajisi" (Marko 7:21-23).
Paulo: "Basi matendo
ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, ugomvi, wivu, hasira,
fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana
na hayo; katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia,
ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme
wa Mungu" (Wagalatia 5:19-21).
Biblia yaeleza mwanzo wa dhambi za mwanadamu kuanzia
kwa kuanguka kwake katika Edeni, ni kwa kazi ya ukombozi wa Yesu
juu ya Msalaba tu ndio uwezao kuharibu "Ibilisi" huyu.
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo tutakubali pamoja na
Yesu Bwana wetu ukuu wa Mungu Baba; tutaweza kuona Yesu kama mwana
wake mtii, na tutaona Roho Mtakatifu kama nguvu zake mwenyewe:
Paulo: "Mungu ni
mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu
Kristo Yesu" (1 Timotheo 2:5).
Paulo: "Kichwa cha
Kristo ni Mungu" (1 Wakorintho 11:3).
Paulo: "Basi, vitu
vyote vikiisha kutiishwa chini yake, ndipo Mwana mwenyewe naye
atatiishwa chini yake yeye aliyemtiishia vitu vyote, ili kwamba
Mungu awe yote katika wote" (1 Wakorintho 15:28).
Paulo: "Mwili mmoja,
na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito
wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye
ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya
yote" (Waefeso 4:4-6).
Yesu: "Baba ni mkuu kuliko mimi" (Yohana 14:28).
"Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda" (Yohana 5:19).
"Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake" (Yohana 15:10).
"Walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke"
(Luka 22:42).
Malaika Gabrieli:
"Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu
zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho
kitakochozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu." (Luka
1:35).
Petro: "Wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu" (2 Petro 1:21).
"Habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia
mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu" (Matendo 10:38).
Biblia yaelekeza kila kitu kwa Mungu, yaani, Baba;
na nia yote ya Mungu; katika Yesu, yaani, Mwana wa Mungu; na yafunua
kazi ya Mungu katika manabii, mitume na watakatifu kwa nguvu zake
nwenyewe, yaani, Roho Mtakatifu.
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo tutajua kuwa imani
katika Yesu ni lazima. Mkristo anapaswa kukubali injili ya kweli
kabla ya kuwa wa Kristo:
Yesu: "Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele" (Yohana 3:16).
"Kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye,
mtakufa katika dhambi zenu" (Yohana 8:24).
Paulo: "Kwa sababu (injili ya Kristo) ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia" (Warumi 1:16).
"Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako
ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua
katika wafu, utaokoka" (Warumi 10:9).
Waebrania: "Lakini
pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye
Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu
wale wamtafutao" (Waebrania 11:6).
Na, kama onyo kuepuka mafundisho ya uongo:
Paulo: "Lakini ijapokuwa
sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa
hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe" (Wagalatia 1:8).
Au kwa kufuata umati:
Yesu: "Ingieni kwa
kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia
ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo.
Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao
waionao ni wachache" (Mathayo 7:13).
Biblia haituruhusu kuchukulia wokovu kama jambo
hivi hivi. Njia ya pekee kwa wenye dhambi ni kufuata katika utii
ambao Yesu ameongoza, kwa imani katika yeye na katika Neno la
Mungu aliloliheshimu.
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo tutapenda kuudharau
unyonge na kiburi cha maumbile yetu ya kimwili, na kuyaweka chini
kama alivyofanya Yesu katika kifo chake juu ya Msalaba:
Yesu: "Mtu ye yote
akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake,
anifuate" (Mathayo 16:24).
Paulo: "Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwemo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye . . . alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkarimia Jina lile lipitalo kila jina" (Wafilipi 2:5-11).
"Utu wetu wa kale ulisulubishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike" (Warumi 6:6).
"Nimesulubiwa pamoja na Kristo lakini ni hai; wala sisimami tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu" (Wagalatia 2:20).
Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake" (Wagalatia 5:24).
Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote
ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu
umesulubiwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu" (Wagalatia 6:14).
Yesu: "Hao ndio . . . wamefua mavazi yao, na
kuyafanya meupe katika damu ya Mwanakondoo" (Ufunuo 7:14).
Kwa mauti yake juu ya Msalaba, Yesu aliharibu nguvu
za dhambi, na sasa yu mkamilifu na aishi milele. Wale wanaosulubisha
maisha yao ya zamani na Kristo na wanaotaka Kumfuata, watapokea
msaada wake kwa njia hiyo.
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo tutajua kuwa twapaswa
kutii amri ya Yesu, tufuate imani yetu kwa ubatizo:
Yesu: "Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote . . . Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini . . . na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninaye pendezwa naye" (Mathayo 3:15-17).
"Aaminiye na kubatizwa ataokoka asiyeamini, atahukumiwa" (Marko 16:16).
"Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi
kuuingia ufalme wa Mungu" (Yohana 3:5).
Petro: "Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu" (Matendo 2:38).
"Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa
Wakawa
wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika
kuumega mkate, na katika kusali" (Matendo 2:41, 42).
Paulo: ". . . sisi
sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti
yake. Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti
yake" (Warumi 6: 3, 4).
Katika Biblia, ubatizo (kuzikwa majini), hufanywa
na wale ambao wamekiri tamaa yao ya kusulubisha na kuzika maisha
yao ya awali, na waanze upya tena katika maisha mfano wa ufufuo
wa Kristo.
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo tutapenda Kufuata mfano
wa maisha ya Yesu, kulinda amri zake, kukumbuka mauti yake, na
kujitenga na ulimwengu:
Yesu: "Mkinipenda, mtazishika amri zangu" (Yohana 14:15).
"Amri mpya nawapa, Mpendane" (Yohana 13:34).
"Rudisha upanga wako mahali pake; maana wote
waushikao upanga, wataangamia kwa upanga" (Mathayo 26:52).
Yohana: "Msipende
dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia . . . Maana kila kilichomo
duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha
uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia" (1 Yohana
2:15, 16).
Paulo na Yesu:
"Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa
nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa aliutwa mkate,
naye akiisha kushukuru akaumega akasema, huu ndio mwili wangu
ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi
hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, kikombe hiki ni
agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa
ukumbusho wangu" (1 Wakorintho 11:23-26).
Kwa hivyo Biblia yawapa nguvu Wakristo wa kweli
kumkumbuka Bwana katika kuumega mkate kila mara, na wapate kumkumbuka
bila kukoma katika maisha yao, wakingoja kwa hamu kuja kwake mara
ya pili.
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo tutafahamu kuwa siku moja tutasimama mbele ya Yesu Kristo kama Hakimu wetu, ili tupokee baraka au laana:
Yesu: "Kila neno
lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno
hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki,
na kwa maneno yako utahukumiwa" (Mathayo 12:36, 37).
Paulo: "Kwa maana
imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha
Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili,
kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya" (2 Wakorintho
5:10).
Danieli: "Tena, wengi
wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate
uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele" (Danieli
12:2).
Yesu: "Hasira yako
nayo ikaja, na wakati ukaja wa kuhukumiwa waliokufa, na kuwapa
thawabu yao watumwa wako manabii na watakatifu, na hao walichao
jina lako, wadogo kwa wakubwa na wa kuwaharibu hao waiharibuo
nchi" (Ufunuo 11:18).
Paulo: "Kutakuwa na ufufuo wa wafu, wenye haki na wasio haki pia" (Matendo 24:15).
Alipokuwa akitoa hoja zake katika habari ya haki,
na kuwa na kiasi, na hukumu itakayokuja, Feliki akafanya hofu"
(Matendo 24:25).
Petro: "Nao (waendao
kwa tamaa za wanadamu) watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari
kuwahukuma walio hai na waliokufa" (1 Petro 4:5).
Wale ambao wamefahamu Ukweli wa Mungu, kama wamekubali
na kuamini au kutoamini, kukataa au kudharau, watalazimika kusimama
mbele ya kiti cha Bwana cha hukumu, kwa baraka au kwa laana.
Yesu: "Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu . . . Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake" (Mathayo 25:31-46).
"Ni afadhali kuingia katika kuzimu u kigutu,
kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto
usiozimika" (Marko 9:43-48).
Jehanum (hell) ya Biblia ni kuharibiwa kwa kila
kitu kisichopendeza machoni pa Mungu wakati wa hukumu. Pia huitwa
"moto wa milele" na "ziwa la moto."
Ikiwa twajidai kuwa Wakristo twaweza kutazamia wakati
ambapo dunia itatakaswa katika kazi ya Kristo, na kujawa na utukufu
wa Mungu:
Kwa Musa: "Lakini hakika yangu, kama niishivyo, tena kama dunia hii nzima itakavyojawa utukufu wangu" (Hesabu 14:21).
"Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako, na mwana wa mfalme haki yako. Atawaamua watu wako kwa haki, na watu wako walioonewa kwa hukumu" (Zaburi 72:1, 2)
"Na ahihimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, atendaye
miujiza Yeye peke yake; Jina lake tukufu na lihihimidiwe milele;
dunia na ijae utukufu wake" (Zaburi 72:18, 19).
Isaya: "Hawatadhuru
wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia
itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari"
(Isaya 11:9).
Habakuki: "Kwa maana
dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa Bwana, kama maji yaifunikavyo
bahari" (Habakuki 2:14).
Paulo: "Hapo ndipo
mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala
wote, na mamlake yote, na nguvu. Maana sharti amiliki yeye, hata
awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake. Adui wa mwisho
atakayebatilishwa ni mauti" (1 Wakorintho 15:24-26).
Yesu: "Mauti na kuzimu (kaburi) zikatupwa katika lile ziwa la moto" (Ufunuo 20:14)
Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu,
naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake.
Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kila chozi
katika macho yao, wala mauti haitakuwepo tena; wala maombolezo,
wala kilio, wala maumivu hayatakuwepo tena; kwa kuwa mambo ya
kwanza yamekwisha kupita" (Ufunuo 21:3, 4).
Hivi Biblia yaonyesha jinsi ukamilifu uliokusudiwa katika kazi ya uumbaji utaonekana, kwa wote walio watakatifu wa kweli wa Mungu.
Wale wanaotaka kuchunguza zaidi juu ya mambo haya
waweza kupata msaada tayari kutokana na vitabu na vijitabu vipatikanavyo
kutoka kwa: